Jumatano , 12th Dec , 2018

Jumla ya klabu 15 kutoka mataifa 7 barani Ulaya tayari zimeshakata tiketi ya kucheza hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa barani humo huku ikiwa imebaki nafasi moja tu kukamilisha timu 16.

Mpira maalum unaotumika kwenye ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Nafasi hiyo inawaniwa na timu mbili kutoka mataifa ya Ufaransa na Ukraine ambayo yanawakilishwa na klabu za Shakhtar Donetsk ambao watakuwa wenyeji wa Olympique Lyonnais leo kwenye mchezo wa kundi F.

Katika mchezo huo utakaopigwa leo kuanzia saa 5:00 usiku, wageni Olympique Lyonnais wenye alama 7 wanahitaji sare ya aina yoyote ili wafuzu hatua ijayo wakati wenyeji Shakhtar Donetsk  wenye alama 5, wanahitaji ushindi.

Katika timu ambazo tayari zimeshafuzu, Uingereza imeongoza kwa kuingiza timu 4 amabazo ni Manchester United, Manchester City, Liverpool na Tottenham. Hispania na Ujerumani kila mmoja zimeingiza timu 3.

Timu za Hispania ni mabingwa watetezi Real Madrid, Barcelona na Atletico Madrid wakati Ujerumani ni Bayern Munich, Borussia Dortmund na Schalke 04.

Mataifa mengine ni Italia iliyoingiza timu mbili, AS Roma na Juventus, wakati Ureno imeingiza Porto na Uholanzi imeingiza Ajax. Ufaransa imeingiza PSG lakini ina nafasai leo ya kuingiza timu mbili endapo Lyon itaifunga Shakhtar Donetsk.